Ilikuwa ni mida ya saa kumi na moja jioni mitaa ya tabata mawenzi, siku hiyo tukiwa na rafiki yangu Pascal Itangaja tukiwa ndani ya suti kali nyeusi .Tulikuwa tukitembea kuelekea kituo cha daladala ili kuwahi mkutano wa ‘Leadership & Lifestyle Forum’ pale Serena Hotel zamani ‘Movenpick Hotel’ tuliokuwa tumealikwa na rafiki yetu mmoja kutoka Nigeria aitwaye Obafemi Banigbe. Kwakweli tulikuwa tumetokelezea haswa ingawa mifukoni tulikuwa na elfu moja tu ya nauli na hakuna aliyejua. Vijasho vyembamba vilikuwa vinatutoka kwa sababu ya jua la jioni na barabarani tulikutana na watoto wadogo wakicheza mpira na tulipotokea ghafla walisimama wakaanza kuitana kwa nguvu. “ Simamisha mpira simama wachungaji wanapita” . Tulitabasamu na kuendelea na safari kama kawaida.
Hiyo ilikuwa ni mwaka 2007 miaka miwili tu baada ya kumaliza chuo kikuu cha Dar es Salaam na kujikuta tukipambana mtaani baada ya jitihada za ujasiriamali kushindikana. Mimi pamoja na rafiki zangu wengine tulishindwa kusimamisha gazeti tuliloanzisha na kujikuta tukikosa hata pesa ya kula huku tumezungukwa na madeni lukuki na mbele yetu tukiona kiza kikuu. Wote tulikuwa tumekata tamaa ya maisha , tulikuwa tumechoka maisha ya kuungaunga na mahangaiko ya gheto. Tulitamani siku moja tupate kazi ya kueleweka, tujenge nyumba zetu na tumiliki japo gari la mkopo. Lakini pamoja na matatizo yote hayo bado ndani yetu tuliamini kuwa uwezo tunao. Tulijua kuwa hatubabaishi na kuwa ipo siku moja milango itafunguka. Ingawa soli zetu za viatu zilikuwa zimekwisha na njaa ilikuwa ni kali, bado kitu fulani ndani ya mioyo yetu kilisema inawezekana, hivyo tulisonga mbele.
Wakati huo tayari tulikwisha sajili kampuni mbili kwa jina la East Africa Speakers Bureau (EASB) na National Tour Operator Limited (NATOL). Lakini mwanzo ulikuwa mgumu sana kwani hatukuwa na ofisi wala pesa ya kufanyia biashara hivyo ofisi ilikuwa pale tulipokuwepo kwa wakati uliokuwepo. Kimsingi ofisi yetu ilikuwa ni vichwa vyetu. Ni kipindi hichohicho nilipokuwa na mawazo ya kufunga ndoa na mke wangu mpendwa Lilian John Msacky ingawa sikuwa nimejiandaa vya kutosha hivyo nilifanya maamuzi magumu ya kuoa nikiamini Mungu atakuwa pamoja na familia yangu. Wakati tukiwa ‘honeymoon’ pale Regency Hotel, Mikocheni karibu na kituo cha basi cha Mwl. Nyerere, usiku wa harusi, nilipigiwa simu yapata saa kumi na mbili asubuhi ya kwamba kuna wateja wanataka kukodisha magari . Nakumbuka huo ndio ulikuwa mwisho wa Honey Moon kwani mimi na mke wangu hatukuwa na gari hata moja hivyo tuliamka kwenda kutafuta vocha za simu kwenye vibanda pembezoni mwa barabara na kuanza kuwapigia simu watu wenye magari waweze kukagulisha kwa ajili ya kukodiwa. Nakumbuka tulikuwa na ‘counter book’ yenye majina ya watu wanaomiliki magari mbalimbali hapa mjini. Kwa vile hatukiwa na mtaji wa biashara, ilitulazimu kutumia ela kidogo ya zawadi kutoka kwenye kamati ya harusi kuwapa wenye magari ela ya mafuta ili waje kukagulisha magari. Kwa bahati mbaya ile biashara hatukuipata kwani wengi wa wenye magari walikuwa watu wenye uwezo na hawakupenda kusumbuliwa asubuhi ile na wengi walisema wamepumzika na familia zao tusiwasumbue asubuhi asubuhi. Kwa kweli haikuwa rahisi kama unavyoweza kufikiria lakini huo ndio ulikuwa mwanzo wa ujasiriamali miaka mitano tu iliyopita. Na leo ninashuhudia mwenyewe namna NATOL inavyokuwa kadri Mungu anavyotubariki.
Yamkini leo hii unapitia magumu kuliko haya unayoyasoma na umeanza kukata tamaa kwa sababu vitu havitokei kama ulivyotarajia. Inawezekana kabisa kila mtu anakucheka na kukusimanga kwamba umepotea njia kwa sababu hueleweki. Kama mwanadamu yeyote ni lazima unajisikia vibaya na kuanza kujiuliza maswali mengi kuhusu maamuzi uliyoyafanya. Pengine ndiyo kwanza umeamua kushiriki katika uchaguzi wa kisiasa na kura hazijatosha. Unaona aibu na unajuta kwa nini uliamua kushiriki. Tambua kuwa dunia hii ina mambo mengi ya kukatisha tamaa na hakuna mwanzo mrahisi. Siku zote nikitizama maisha ya watu mbalimbali waliopiga hatua katika maisha nagundua ya kwamba wamepitia changamoto nyingi sana. Nikitizama historia ya watu kama Opra Winfrey nagundua kwamba mimi nina nafuu mara mia moja. Hebu fikiria maisha ya mzee Nelson Mandela aliyekaa jela miaka ishirini na saba? Hebu fikiria kukaa jela kwa zaidi ya umri wa mtu mzima! Hebu fikiria kiongozi kama Abraham Lincoln ambaye alishindwa uchaguzi mara kadhaa kabla ya kuwa rais wa heshima katika historia ya Marekani! Hebu fikiria jinsi Barack Obama alivyoshindwa uchaguzi mara tu alipoingia katika siasa, vipi kama hawa wangekata tamaa? Wangefika hapo walipofika?
Changamoto unazopitia leo hii ni mchakato wa kukuimarisha na kukupa uzoefu wa kumudu mikikimikiki ya maisha. Unayopitia leo yanakuimarisha na kukuandaa kwa mambo makubwa hapo mbele. Ili kwamba utakapofanikiwa katika ndoto yako uweze kudumu na kupanda zaidi. Changamoto za maisha zinajenga nidhamu na kukupa maarifa ya kuishi katika hali ya shida na raha. Usijali nini watu wanasema kuhusu wewe na usijali nini wenzako wanafanya. Ni kawaida kwa binadamu kusema, huwezi kuwazuia watu kusema na watendelea kusema bila kujali uko katika shida au neema. Jambo la msingi kwako ni kumtanguliza Mungu na kusimama katima maono uliyonayo. Nchi yetu bado ina fursa na rasilimali nyingi. Ushindani katika nyanja nyingi bado ni mdogo ukilinganisha na nchi zilizoendelea. Kwa mtazamo huo bado kuna fursa kwa wewe kuwa ni miongoni mwa watanzania waliofanikiwa katika ndoto yako. Sikiliza moyo wako unataka kufanya nini na bila kujali ulichonacho mkononi iwe ni mtaji au msaada anza kufanyia kazi ndoto yako kidogokidogo. Akili yako yote iangalie wapi unaelekea na si wapi ulipo sasa. Mawazo yako yaamini kuwa ipo siku moja utakuwa ni mtu wa kutolewa mfano katika fani yako na pengine utatengeneza ajira kwa watanzania wenzako.
Usipoteze muda wako kusikiliza maneno ya kukatisha tamaa. Kuwa makini na aina ya marafiki unaotengeneza, kuwa makini na aina ya vitu unavyovisoma na kuvisikiliza. Soma historia za watu waliofanikiwa katika fani yako, tafuta taarifa kuhusu jambo unalotaka kulifanya iwe ni biashara au ugunduzi wa kisayansi na kila siku fanya kitu fulani cha kukusogeza mbele kuelekea katika ndoto yako. Ni kweli hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi na njiani utakutana na milima na mabonde. Utakuwa na vipindi vya kuchoka na kukata tamaa lakini hapo ndipo unapotakiwa kuongeza bidii. Nakumbuka msemo wa kaka yangu Eric siku zote amekuwa akiniambia kuwa ‘maji umeshayavulia nguo na ni kwamba uko kisiwani na umeshachoma mashua kurudi nyuma huwezi kilichobaki ni kupambana ubakie kisiwani vinginevyo uliwe na wanyama wa mwituni’. Falsafa hii imekuwa ni kama wimbo wa simu ‘ringtone’ ndani ya kichwa changu na siku zote ninapokuwa naelekea kukata tamaa nakumbuka kuwa niko kisiwani kwenye wanyama wakali na kuna mawili ‘nifanye bidii ili niendelee kuishi au nikate tama na kuliwa na wanyama’ . Nianapowaza hilo tu napata nguvu mpya ya kuendelea kutafuta katika maisha.
Ndugu yangu, shukuru Mungu kwamba amekupa uhai na nguvu ya kufanya kazi. Shukuru Mungu kwamba amekupa nafasi ya kusoma makala hii na kupata nguvu mpya. Haujakutana na makala hii kwa bahati mbaya. Hii ilikuwa ndani ya mpango mzima wa maisha yako kwamba ipo siku utasoma maandiko yatakayokutia moyo kwa sababu ndoto yako ni halisi wala si ndoto ya alinacha. Nakusihi uamini na usikilize sauti itokayo ndani ya moyo wako isemayo piga moyo konde na songa mbele. Ipo siku utasahau yote haya na yatabaki kuwa historia. Utakuwa umejisaidia wewe mwenyewe, familia yako, watanzania wenzako na kizazi chako chote. Natamani siku moja upate kazi, au biashara au uongozi sawasawa na ndoto yako. Leo uko mlimani lakini tambua kuwa mbele ya kila mlima kuna mteremko. Usikate tamaa, yote yanawezekana

No comments:
Post a Comment